Mambo ya Walawi. Chapter 12

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na hao wana wa Israeli, uwaambie, Mwanamke akitunga mimba na kuzaa mtoto mume, ndipo atakuwa yu najisi siku saba; kama katika siku za kutengwa kwake kwa ajili ya hedhi, ndivyo atakavyokuwa najisi.
3 Siku nane mtoto atatahiriwa govi ya zunga lake.
4 Na huyo mwanamke atakaa katika damu ya kutakata kwake siku thelathini na tatu; asiguse kitu kilicho kitakatifu, wala asiingie mahali patakatifu, hata siku hizo za kutakata kwake zitakapotimia.
5 Lakini kwamba amezaa mtoto mke ndipo atakuwa najisi juma mbili, kama katika kutengwa kwake; naye atakaa katika damu ya kutakata kwake muda wa siku sitini na sita.
6 Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mwana, au kwa ajili ya binti, ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani;
7 na yeye atawasongeza mbele za Bwana, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika na jicho la damu yake. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, kwamba ni mtoto mume au mke.
8 Kama mali yake huyo mwanamke haimfikilii mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.